Watatu mbaroni kwa kuchimba mahandaki bila kibali

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Evance Ndeka Bisesagu (47), mfanyabiashara na mkazi wa Bupumula, Kata ya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela, kwa tuhuma za kuchimba mahandaki sita na kufanya shughuli za ujenzi wa nyumba ya makazi bila kufuata taratibu za kisheria.


​Mtuhumiwa huyo, ambaye ni mmiliki wa jengo hilo, amekamatwa tarehe 22.04.2026 majira ya jioni kufuatia taarifa za wananchi kuhusu uwepo wa mahandaki hayo yanayohatarisha usalama wao ambapo  baada ya ufuatiliaji wa kina imebainika kuwa mtuhumiwa alikuwa akijihusisha na shughuli za ujenzi wa mahandaki bila kuwa na vibali vyovyote kutoka mamlaka husika, wala kutoa taarifa kwa mamlaka za kisheria.

​Pamoja na mmiliki huyo, Jeshi la Polisi linawashikilia watu wengine wawili ambao ni Ngasa Kasuka na Hamad Juma Kashinje, ambao ni vibarua waliokuwa wakishiriki katika shughuli za ujenzi katika eneo hilo huku msako ukiendelea kuwatafuta mafundi na watu  wengine waliokuwa wakishirikiana nao katika ujenzi na uchimbaji wa mahandaki hayo.

Aidha, ​Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kutoa rai kwa viongozi wa mamlaka mbalimbali za Serikali kufuatilia kwa kina mienendo ya watu wanaoishi katika maeneo yao ili kujiridhisha na usalama. 


Vilevile, kwa ujenzi wowote unaofanyika katika mitaa hiyo, mamlaka zinazohusika na ujenzi zinatakiwa kuhakikisha kuwa vibali vinazingatiwa; na yeyote atakayebainika kujenga bila vibali, shughuli hizo lazima zisitishwe.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii