ATHARI mbaya za kusitishwa kwa huduma za matibabu ya punda katika kituo cha kipekee kilichoko kisiwani Lamu tayari zimeanza kushuhudiwa, wakazi wakikosa namna ya kutibu wanyama hao.
Wakati ambapo ulimwengu mzima una wasiwasi kuhusu uhaba wa mafuta utakaosababishwa na vita vya Mashariki ya Kati, hali itakayoathiri sana uchukuzi, wakazi wa Lamu wana wasiwasi kuhusu athari zitakazosababishwa na kufungwa kwa kituo cha matibabu ya punda.
Katika kisiwa hicho, punda ndio hutegemewa zaidi kwa uchukuzi wa watu na mizigo.
Ijumaa iliyopita, usimamizi wa kituo cha matibabu ya punda kilicho kisiwani uliweka notisi ya ghafla kuijulisha jamii ya Lamu kwamba imesitisha huduma zake.
Hatua hiyo ilichukuliwa kupisha ukarabati na ujenzi wa jumba la ofisi zake ambalo lina nyufa.
Bw Mahmoud Suleiman Hamid, mkazi wa Bajuri kisiwani Lamu, anasema punda wake hajakuwa akila chochote kwa karibu siku sita sasa.
Hilo linatokana na matatizo ya tumbo, shida ya kupumua na majeraha mengi ya mwili ambayo mnyama wake anauguza.
“Tunapata shida zisizokadirika kwa kukosa tiba ya punda hapa kisiwani. Nimekuja hapa hospitali ya punda nikitumia pikipiki.
“Najua kumfunga mnyama namna hii haifai. Ila nimelazimika kufanya hivyo angalau nifike hapa haraka ilmuradi niokoe maisha yake.
“Mnyama huyu yuko mahututi. Kituo nacho kimefungwa. Nahofia kumpoteza punda wangu,” akasema Bw Hamid.
Aliwaomba wasimamizi wa kituo cha matibabu ya punda kubuni mbinu mbadala na za haraka kuwasaidia wenye punda wakati wakiendelea kukarabati jumba lao.
“Tumezoea tukija hapa na punda mahututi wanalazwa. Leo hii hata kuhudumiwa na kutoka na punda wetu bado hakufanyiki. Warejeshe huduma haraka. Ikiwa wamefunga kabisa na kuondoka kisiwani pia watujulishe,” akasema Bw Hamid.
Bw Ali Salim, mkazi, alisikitika kuwa tangu huduma zisitishwe, kuna baadhi ya wenye punda ambao tayari wamepoteza wanyama wao.
“Ukipita mitaani pia utapata punda wakilala na kuugua bila usaidizi. Punda ni kiungo muhimu kwetu. Matibabu yao yazingatiwe bila kukatizwa,” akasema Bw Salim.
Mtetezi wa Maslahi ya Punda, Kaunti ya Lamu, Bi Jamila Mitsanze aliiomba serikali ya kaunti hiyo kujenga kituo cha umma cha matibabu ya punda ili kusaidia kile kilichoko sasa ambacho ni cha kibinafsi.
Pia aliwashauri wenye punda kuunda vyama vya ushirika ili kujisaidia wanapokumbwa na matatizo.
Daktari Msimamizi wa Kituo cha Matibabu ya Punda Lamu, Bw Obadiah Sing’oei, alisema wamepanga mkutano na wadau wengine pamoja na jamii ili kutafuta namna ya kuendeleza huduma wanaposubiri ukarabati wa jengo ufanywe.
Kauli yake iliungwa mkono na Mkurugenzi wa Masuala ya Matibabu ya Mifugo wa Kaunti ya Lamu Felix Rachuonyo, aliyesisitiza haja ya wananchi kuondoa shaka kwani tatizo lililopo linashughulikiwa.
“Tuna maafisa wetu zaidi ya 10 wanaoshughulikia matibabu ya mifugo, wakiwemo punda mjini Lamu na Shella. Tutasaidiana na kituo cha matibabu ya punda ili huduma ziendelee wakati tatizo likishughulikiwa. Hakuna la kuhofisha,” akasema Bw Rachuonyo.