HOSPITALI ya Rufaa ya Kaunti ya Kericho imehifadhi miili 49 ambayo ni mara tatu zaidi ya idadi yake ya kawaida, hii ikizua tatizo la afya ya umma.
Hii ni baada ya miili 33 ambayo ilizikwa kisiri Makaburini mjini Kericho kufukuliwa mnamo Jumanne na kuhifadhiwa hospitalini humo.
Kwa mujibu wa Dkt Richard Njoroge, Mwanapatholojia wa Serikali, kati ya miili hiyo 25 ni ya watoto huku minane ikiwa ya watu wazima.
Awali polisi walikuwa wamesema miili ambayo ilizikwa kwenye kaburi la kina kifupi ilikuwa 14.
Hata hivyo, baada ya kufukuliwa, ilipatikana miili ilikuwa 33 na sehemu sita za viungo vya mwili.
“Mochari hii ina uwezo wa kusitiri miili 16 lakini sasa tuna 49 na sehemu sita za viungo vya mwili,” akasema afisa wa ngazi ya juu kwenye Idara ya Afya ya Serikali ya Kaunti ya Kericho jana.
Alifichua kuwa wakati ambapo miili hiyo ilikuwa inaletwa kwenye hifadhi hiyo, tayari mochari ilikuwa imejaa.
“Ilibidi nafasi itengewe miili 33 mipya kwa kuondoa ile iliyokuwa kwenye jokofu. Tuna imani familia zao zitajitokeza na kuichukua kwa muda mfupi ili kuzuia isiharibike,” akasema afisa huyo wa afya.
Kufikia jana, miili 16 iliyokuwa kwenye mochari hiyo awali haikuwa imechukuliwa wala hakuna mingine iliyokuwa imeletwa mbali na ile iliyokuwa imefukuliwa.
Kutokana na kusafirishwa kwa miili iliyofukuliwa hadi Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kericho, uvundo mkali ulikuwa umeanza kuhisiwa kwenye barabara ya Kisii-Kericho.
Hospitali hiyo ni wazi kwa umma na hifadhi ya maiti imetenganishwa tu na barabara kupitia kuta zilizoezekwa kwa mabati.
Dkt Njoroge akiwa ameandamana na Mkuu wa Kitengo kinachohusika na uchunguzi wa vifo katika Idara ya Upelelezi nchini (DCI), Dkt Martin Nyaguto na Kamishna wa Kaunti Gicheru Mwai, alisema baada ya kufukuliwa kwa miili hiyo sasa uchunguzi wa maiti ndio utafuata.
“Baadhi ya miili ilikuwa bado sawa lakini mingine ilikuwa imefika hatua tofauti ya kuharibika. Hii inaonyesha kuna ile iliyotoka mochari na pia nyakati walizoaga dunia zilikuwa tofauti,” akasema Dkt Njoroge.
“Uchunguzi wa postmortem ni mchakato mzima na tena utafanyika kwa makini kwa hivyo hatuwezi kujua upasuaji utachukua muda upi,” akaongeza.
Mahakama ya Kericho mnamo Jumatatu ilikuwa imetoa amri kwa DCI ifukue miili hiyo kwa ajili ya uchunguzi.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime