Mkenya ashtakiwa nchini Namibia kwa mauaji ya mpenzi wake

Mwanaume mwenye umri wa miaka 40, amejipata mashakani baada ya kushtakiwa kwa mauaji ya mpenzi wake, raia wa Namibia nchini humo.

Geoffrey Jeff Kasume alirushwa rumande baada kuwasilishwa mbele ya Korti ya Hakimu Katutura katika jiji kuu la Windhoek, ambapo alishtakiwa rasmi kwa mauaji ya Regina Nambashu Kondombolo, 33.

Upande wa mashtaka ulifanikiwa kupinga mshukiwa kuachiliwa kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea kuhusu mauaji hayo.

Kulingana na nakala ya kesi iliyowasilishwa kortini, mnamo au karibu na Februari 7, 2026, Bw Kasume “alimuua Kondombolo kinyume cha sheria na kimaksudi makazini mwake eneo la Otjomuise Extension 2.”

Serikali ya Namibia imechukulia suala hilo kuwa mauaji kuambayana na vifungu vya Sheria ya Namibia kuhusu Dhuluma za Kinyumbani, ikihoji kuwa mshukiwa na marehemu walikuwa katika uhusiano wa kimapenzi tukio hilo lilipotokea.

Nakala za korti zinawataja wawili hao kuwa wapenzi.

Mwendeshaji Mashtaka Tatelo Cuthbert Lusepani alipinga ombi la mshukiwa kuachiliwa kwa dhamana akisema uchunguzi ungali katika hatua za mwanzomwanzo.

Kumwachilia Kasume, alihoji, huenda kukahujumu mahojiano yanayoendelea na kutatiza mashahidi au ushahidi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii