Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, Februari 26, 2026 amezindua mafunzo ya maadili kwa viongozi na watumishi wa umma mkoani humo, yanayotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akifungua mafunzo hayo, Mhe. Mtanda amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utekelezaji wa majukumu ya umma ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa uadilifu.
Ameonya dhidi ya rushwa, migongano ya maslahi na maamuzi yanayokiuka sheria, akieleza kuwa kukosekana kwa maadili kunadhoofisha juhudi za maendeleo.
Aidha, amewapongeza watumishi wanaowasilisha tamko la mali kwa wakati na kuwataka wengine kuzingatia wajibu huo kisheria.
Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Sekretarieti hiyo Kanda ya Ziwa, Bw. Godson Kweka, amesema mafunzo hayo yanawalenga viongozi kuwakumbusha matakwa ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ikiwemo uwajibikaji na utoaji wa tamko la mali.
Hata hivyo amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, matamko 2,000 yamewasilishwa Kanda ya Ziwa, huku Mwanza ukiongoza kwa uwasilishaji wa wakati. Pia, kati ya malalamiko 16 yaliyopokelewa, 11 yalitoka Mkoa wa Mwanza.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime