Bima ya Afya kwa Wote: Kitita Maalumu Kuanza Rasmi Kesho

Wananchi wasio na uwezo nchini sasa wana sababu ya kutabasamu kufuatia kuanza rasmi kwa kitita cha huduma muhimu chini ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, hatua inayolenga kupanua wigo wa upatikanaji wa matibabu kwa makundi maalumu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 25, 2026 na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, kaya yenye watu wasiozidi sita itachangia Sh150,000 kwa mwaka na kunufaika na huduma hizo. Wanufaika ni pamoja na wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, ambapo kaya itahusisha mwanachama mchangiaji, mwenza wake na wategemezi wanne.

Aidha huduma zitakazotolewa kupitia kitita hicho kinachoanza Februari 26, zinajumuisha usajili na kulazwa katika wodi za kawaida, ushauri wa kitabibu, vipimo zaidi ya 80 vya maabara na radiolojia, pamoja na dawa na vifaa tiba 247 kwa magonjwa ya kawaida na sugu. Aidha, huduma 36 za upasuaji mdogo na mkubwa zitatolewa, ikiwemo uzazi na upasuaji wa dharura.

Hata hivyo utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya ahadi ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, ambapo aliahidi kuzindua Bima ya Afya kwa Wote ndani ya siku 100 na kuanza na makundi maalumu.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii