Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imekamilisha ujenzi wa nyumba mbili pacha za askari Polisi katika Mtaa wa Mgusu, Kata ya Mgusu, Wilaya ya Geita mkoani Geita, hatua inayolenga kuboresha makazi ya askari na kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo hilo.
Ujenzi wa nyumba hizo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 77, fedha zilizotumika kukamilisha maboma yaliyoanzishwa awali kwa nguvu za wananchi, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano kati ya jamii, wadau wa maendeleo na GGML.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi nyumba hizo kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Kaimu Mkurugenzi wa GGML, Duan Campbell, amesema mgodi huo haujajikita tu katika uchimbaji wa dhahabu bali pia katika kuchangia maendeleo ya kijamii.
Duan amesema mradi huo unaimarisha mahusiano kati ya mgodi na jamii pamoja na kuongeza ufanisi wa ulinzi na usalama katika maeneo yanayozunguka mgodi na makazi ya wananchi.
“Sera ya GGML inaamini kuwa jamii imara hutegemea taasisi imara. Moja ya taasisi muhimu katika ustawi wa jamii ni Jeshi la Polisi. Askari wanapopata makazi bora, utulivu wao na uwezo wa kutumikia wananchi huongezeka,” amesema Duan.
Ameongeza kuwa usalama hauishii ndani ya mgodi pekee bali pia majumbani, barabarani, shuleni na mitaani ambako wananchi wanaishi na kufanya kazi.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mgusu, Nazoro Marcel, amesema mradi huo ulianza mwaka wa fedha 2019/2020 kupitia nguvu za wananchi na wadau wa maendeleo, ambapo walijenga msingi na maboma kwa thamani ya shilingi milioni 19 kabla ya GGML kuendelea na hatua za ukamilishaji.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, amesema ushirikiano kati ya wananchi, wadau wa maendeleo na Serikali umeleta mafanikio katika kupunguza matukio ya uhalifu mkoani humo, akitaja GGML kuwa mdau muhimu wa amani na usalama.
Kamanda Jongo amesema mchango wa GGML umeboresha mazingira ya kazi ya askari na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za kiusalama kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, ameipongeza GGML kwa msaada huo na kuiomba kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutenga bajeti ya ujenzi wa kituo bora cha Polisi katika Kata ya Mgusu ili kukidhi mahitaji ya eneo hilo.
Kwa taarifa zaidi tufuatilie na usikilize jembe Habari Kamili hapo saa moja kamili jioni ambapo msomaji wetu wa hii leo ni Evance Mlyakado tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.
Lakini pia tembelea mitandao yetu ya kijamii ya Jembefmtz
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime