Rais Kiir Amteua Marehemu Kwenye Kamati ya Uchaguzi

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit amejikuta katika sintofahamu baada ya kumteua kimakosa mtu aliyeshafariki dunia kuwa mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Uchaguzi wa taifa hilo.

Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu kulikuwa na mkanganyiko wa kiutawala wakati wa mchakato wa uteuzi, hali iliyosababisha jina la Steward Sorobia Budia, aliyekuwa mwanasiasa wa upinzani, kujumuishwa katika amri ya rais ilhali Budia alifariki dunia takribani miaka mitano iliyopita.

Taarifa zinaeleza kuwa kosa hilo limezua mjadala mkubwa ndani ya nchi, huku familia ya marehemu ikidai fidia kwa kile ilichokiita kukiukwa kwa mila na tamaduni zao.

Familia imesema kuwa katika jamii yao, ni marufuku kumtaja, kumhusisha au “kuamsha” roho ya marehemu bila ridhaa na ushiriki wa wanafamilia, na kwamba hatua hiyo imewaumiza kisaikolojia na kijamii.

Aidha tukio hilo linakuja wakati Sudan Kusini ikiendelea kujiandaa na uchaguzi wa kwanza wa kitaifa tangu ipate uhuru mwaka 2011, baada ya miaka mingi ya migogoro ya kisiasa, vita vya wenyewe kwa wenyewe na changamoto za kiutawala.

Hata hivyo wachambuzi wanasema kosa hilo linaonesha changamoto za kiutendaji ndani ya mifumo ya serikali, hasa katika kipindi nyeti cha maandalizi ya uchaguzi nchini humo.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii