Ajali ya Mashua Ugiriki Yaua Wahamiaji 15 Chios

Watu 15 wamefariki dunia kufuatia ajali ya kugongana kati ya mashua ya walinzi wa pwani ya Ugiriki na mashua iliyokuwa imewabeba wahamiaji, karibu na ufukwe wa Kisiwa cha Chios, nchini Ugiriki.

Kwa mujibu wa taarifa ya mamlaka za Ugiriki iliyotolewa jioni ya jana, hadi sasa miili 15 imeopolewa baharini, wote wakiwa ni wahamiaji. Naibu Meya wa Chios, Pantelis Vroulis, alithibitisha tukio hilo kupitia televisheni ya taifa ya Ugiriki, ERT.

Televisheni hiyo imeripoti kuwa jumla ya watu 25 wamekimbizwa hospitalini katika kisiwa hicho, wakiwemo watoto wadogo 11 pamoja na maafisa wawili wa kikosi cha ulinzi wa pwani.

Katika taarifa za vyombo vya habari zinaeleza kuwa mashua ya wahamiaji ilikuwa imetokea Uturuki ikielekea Kisiwa cha Chios, ikiwa imebeba watu kadhaa waliokuwa wakisaka hifadhi barani Ulaya.

Inaelezwa kuwa ajali hiyo ilitokea wakati mashua ya walinzi wa pwani ilipojaribu kuizuia mashua ya wahamiaji na kuilazimisha kubadili mwelekeo, hali iliyosababisha kugongana baharini.

Kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), takribani wahamiaji 1,000 wameingia katika visiwa vinavyotawaliwa na Ugiriki kwenye Bahari ya Aegean wakitokea Uturuki tangu mwanzoni mwa mwaka huu, hali inayoonesha kuendelea kwa changamoto ya uhamiaji haramu katika ukanda huo.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii