Rais Samia Aanza Mazungumzo ya Kimataifa Dubai Kuvutia Uwekezaji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameanza rasmi mazungumzo na viongozi pamoja na wadau wa kimataifa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja, katika ziara yake ya kikazi jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Katika ratiba ya leo, Rais Samia anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Antigua and Barbuda, Mhe. Gaston Browne, ambapo watajadili masuala ya ushirikiano wa pande mbili, hususan katika nyanja za diplomasia ya kiuchumi na maendeleo.

Aidha, Rais Samia atafanya mazungumzo ya pande mbili na Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism), Bi. Shaikha Al Nuwais, yakilenga kuimarisha sekta ya utalii pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji nchini Tanzania.

Jioni ya leo, Rais Samia anatarajiwa kushiriki uzinduzi wa Global Africa Investment Summit (GAIS), jukwaa la uwekezaji linalolenga kuoanisha miradi iliyo tayari kuwekezeka barani Afrika na wawekezaji wa kimataifa.

Mkutano huo unaendeshwa sambamba na majadiliano ya sera ya World Governments Summit (WGS), ukiwa na dhamira ya kubadili mijadala ya sera kuwa uwekezaji halisi wenye matokeo chanya kwa maendeleo ya Afrika.

Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Tanzania wa kuimarisha diplomasia ya kiuchumi, kukuza ushirikiano wa kimataifa na kuongeza mtiririko wa uwekezaji kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Kwa taarifa zaidi, endelea kutufuatilia na kusikiliza Jembe Habari Kamili saa moja kamili jioni, ikipeperushwa na msomaji wetu wa leo, George Kivumbi.

Pia tembelea  mitandao ya kijamii ya @Jembefmtz.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii