Serikali imeendelea kusisitiza ushirikiano wake na mhimili wa Mahakama kama nguzo muhimu katika kulinda haki, kudumisha amani na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini (Law Day) Kimkoa yaliyofanyika katika Kiwanja cha Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Buswelu, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, yakilenga kuangazia mchango wa Mahakama katika ustawi wa jamii.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya Mahakama na kuboresha mifumo ya utoaji haki ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati.
Mhe. Mtanda amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuimarisha sekta ya haki kupitia ujenzi wa Mahakama pamoja na kampeni ya Mama Samia Legal Aid inayolenga kuwafikia wananchi moja kwa moja.
Amesema kupitia kampeni hiyo, mashauri 1,572 yamesikilizwa, kesi 580 zimekamilika huku kesi 992 zikiendelea, sambamba na utoaji wa elimu ya sheria na huduma za usuluhishi wa migogoro.
Aidha, amesema Serikali imekuwa ikitatua kero katika ngazi za chini ili kupunguza msongamano wa mashauri Mahakamani. Kwa Mkoa wa Mwanza, jumla ya kero 249 zimesikilizwa, kati ya hizo 213 zimekamilika na 36 zinaendelea kufanyiwa kazi.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, amesema Siku ya Sheria ni jukwaa la kutathmini kama haki inatendeka na inaonekana kwa wananchi.
Ameeleza kuwa Mahakama ni mlinzi wa Katiba, mlezi wa haki za raia na ngome ya wanyonge, huku ikichangia maendeleo ya Taifa kupitia amani na utulivu wa jamii.
Amesema katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2025, jumla ya kesi 15,105 zilifunguliwa katika Mahakama za Kanda ya Mwanza, kesi 18,236 zikaamuliwa na kesi 4,086 zinaendelea.
Naye Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Bw. Kabyemela S. Lushagara, amesema Siku ya Sheria ni fursa ya kutafakari wajibu wa Sheria na Mahakama katika kulinda haki, usawa na amani kwa wananchi.
Kwa habari zaidi ungana na Jacob Mlay ambae atatusomea Jembe habari kamili hapo saa Moja kamili jioni
Vilevile tufuatilie kwenye tovuti yetu mahiri kabisa na mitandao yetu ya kijamii @ Jembefmtz
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime