Refa wa kimataifa mwenye historia ya “bahati” kwa klabu za Kaskazini mwa Afrika zinapocheza nyumbani, Tom Abongile kutoka Afrika Kusini, amepangwa kuchezesha mchezo wa Kundi B wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya FAR Rabat ya Morocco na Yanga SC utakaopigwa Februari 7 mwaka huu.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Abongile (34) kusimamia mchezo huo, ikiwa ni mechi yake ya pili katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kuchezeshwa pambano kati ya Esperance ya Tunisia na Stade Malien ya Mali.
Takwimu zinaonesha kuwa timu za Kaskazini mwa Afrika, ambako lugha kuu ni Kiarabu, zimekuwa na matokeo mazuri wanapochezeshwa na Abongile wakiwa nyumbani, mara nyingi zikiibuka bila kupoteza.
Katika mchezo aliochezesha msimu huu kati ya Esperance na Stade Malien, matokeo yalikuwa sare tasa ya 0-0.
Msimu uliopita, Abongile alichezesha michezo minne ya mashindano ya klabu Afrika iliyofanyika Kaskazini mwa Afrika, ambapo wenyeji wote waliibuka na ushindi bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa.
Kwa ujumla, refa huyo tayari amechezesha michezo 12 ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akitoa jumla ya kadi 57 za njano na kadi moja nyekundu, hatua inayoonesha mtindo wake wa kusimamia nidhamu uwanjani.
Hata hivyo uteuzi wake katika mchezo huo unaongeza mvuto na mjadala, hasa kwa mashabiki wa Yanga wanaotazama kwa makini rekodi ya refa huyo katika michezo inayochezwa Kaskazini mwa Afrika.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime