Mwanza Yampongeza Rais Samia kwa Kuimarisha Huduma za Saratani Bugando

Serikali ya Mkoa wa Mwanza imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika sekta ya afya, hususan kuimarisha kitengo cha saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.

Shukrani hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Amir Mkalipa, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saratani kwa Watoto Duniani yaliyofanyika mkoani humo na kuambatana na mchezo wa kirafiki wa mpira wa miguu kati ya timu ya RC na RMO.

Mhe. Mkalipa amesema Rais Samia ameimarisha huduma za matibabu ya saratani kwa kununua mashine kubwa ya mionzi, kupeleka wataalamu kusomea ubingwa na ubingwa bobezi katika masuala ya saratani, kujenga wodi maalum za wagonjwa wa saratani, pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya dawa na vifaa tiba na kuajiri watumishi wapya wa afya.

Aidha, amewashukuru wadau mbalimbali kwa kuendelea kutoa misaada katika matibabu ya watoto wenye saratani, ikiwemo bima za afya na vifaa tiba, huku akiitaka jamii kuendeleza ushirikiano katika kuunga mkono juhudi za Serikali.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba, amewasisitiza wananchi kufuatilia afya za watoto wao mara kwa mara, akieleza kuwa saratani nyingi za watoto hazijulikani chanzo chake lakini zinatibika iwapo zitagundulika mapema na kwa gharama nafuu.

Amesema ni muhimu kubadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi, kula lishe bora, kupata chanjo stahiki, na kupunguza matumizi ya kemikali, mionzi, pombe, sigara na tumbaku ambavyo vinaongeza hatari ya saratani.

Dkt. Lebba pia amesisitiza umuhimu wa bima ya afya kwa wote ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu kwa gharama nafuu na kwa wakati.

Katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Nyamagana, timu ya RC iliibuka na ushindi wa mabao 2–1 dhidi ya RMO.

Aidha, kundi la Veteranas wa Mwanza walichangia vifaa mbalimbali kwa ajili ya watoto wenye saratani.

Sasa ili kupata undani wa  taarifa hii tafadhali usikose kutufuatilie na kusikiliza jembe Habari Kamili hapo saa kumi kamili alasiri ambapo msomaji wetu wa hii leo ni @Florenciapetertz tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.

Lakini pia tembelea mitandao yetu ya kijamii ya Jembefmtz

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii