Watu watano wamefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi kufuatia kuporomoka kwa kingo za udongo (ngema) katika machimbo ya mchanga ya Bolbit, yaliyopo Kijiji cha Makuyuni, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amesema tukio hilo limetokea Februari 15 mwaka huu majira ya saa 11:30 jioni, wakati marehemu hao walipokuwa wakichimba mchanga katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Kamanda Mchunguzi, jitihada za uokoaji zilifanyika kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wananchi wa eneo husika, na kufanikiwa kutoa miili ya watu wote watano kutoka chini ya kifusi.
Aidha Miili hiyo imehifadhiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Korogwe Vijijini, Makuyuni, kwa ajili ya uchunguzi na taratibu nyingine za kisheria.
Waliofariki dunia ni:
Shabani Mrisho maarufu Mwantembo (31)
Yusuph Abdalah maarufu Kibaya
Juma Hatibu maarufu Msikiti (49)
Nurdini Amiri maarufu Daffa (30)
Zamiru Miraji maarufu Daffa (35)
Wote walikuwa wakazi wa Makuyuni, wakijishughulisha na shughuli za kilimo, huku baadhi yao wakifanya pia uchimbaji wa mchanga kama shughuli ya ziada ya kujipatia kipato.
Hata hivyo kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetoa wito kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji kuhakikisha wanazingatia kanuni na misingi ya usalama mahali pa kazi ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha maafa na kuacha familia katika huzuni.
Sasa ili kupata undani wa taarifa hii tafadhali usikose kutufuatilie na kusikiliza jembe Habari Kamili hapo saa saba kamili mchana ambapo msomaji wetu wa hii leo ni @Florenciapetertz tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.
Lakini pia tembelea mitandao yetu ya kijamii ya Jembefmtz
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime