Kesi ya Uhaini ya Tundu Lissu Yaendelea Leo Mahakama Kuu

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, inaendelea leo Jumatatu Februari 16 mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, ambapo shahidi wa saba anatarajiwa kutoa ushahidi wake mahakamani.

Kabla ya kuanza kwa usikilizwaji, maombi mafupi yalifanyika yakiongozwa na dada wa Tundu Lissu, Mchungaji Rose Masesa, aliyemuombea mdogo wake akimtaka Mungu amtie nguvu katika kipindi hiki, na kuwawezesha majaji kutenda haki katika shauri hilo.

Katika usikilizwaji wa Ijumaa iliyopita, mashahidi wawili walitoa ushahidi wao, akiwemo shahidi anayelindwa mwenye umri wa miaka 24, dereva bodaboda anayejitambulisha pia kama mwanachama wa CHADEMA, pamoja na askari mpelelezi Koplo Michael (36), mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro.

Miongoni mwa hoja zilizojitokeza mahakamani ni kubainika kwa tofauti za maelezo kati ya ushahidi uliotolewa mahakamani na taarifa ambazo mashahidi hao walirekodi awali katika vyombo vya uchunguzi.

Itakumbukwa kuwa kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mfululizo kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na mahakama kuu Masjala Ndogo ya DaresSalaam.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii