Makonda Amtaka Msajili Kukamilisha Mchakato wa Mabadiliko Simba

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amemtaka Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Abel Ngilangwa, kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Klabu ya Simba na kutoa majibu rasmi kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kabla ya mwezi huu kuisha.

Makonda ametoa kauli hiyo akisisitiza umuhimu wa kufuata sheria na kanuni katika utekelezaji wa mabadiliko hayo, huku akieleza kuwa kipindi cha uongozi wake kitazingatia kwa umakini misingi ya kisheria katika sekta ya michezo.

“Msajili wa michezo nilitaka mkamilishe taratibu za Simba.

Na nilitaka niwahakikishie kwamba katika kipindi ambacho sheria na kanuni zitafuatwa sana ni hiki cha uongozi wangu,” amesema Makonda.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa Msajili kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuondoa sintofahamu miongoni mwa Wanasimba, akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuona klabu zote nchini zikifanya vizuri na kuendeshwa kwa misingi imara ya kisheria na kiutawala.

“Kamilisha na ikiwezekana kabla ya mwezi huu uwape majibu Wanasimba. Tunachotaka sisi tuone timu hizi zikifanya vizuri. Kabla ya mwezi huu, jambo hili liwe limekamilika,” amesisitiza.

Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na mjadala mpana kuhusu mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji ndani ya Klabu ya Simba, huku wanachama na wadau mbalimbali wakisubiri maamuzi rasmi kutoka kwa mamlaka husika.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii