Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumatano, aliwaongoza viongozi wa serikali, maafisa wa kijeshi na familia za wanajeshi wanne wa nchi yake katika shughuli ya majonzi kutoa heshima za mwisho kwa wanajeshi hao waliouawa katika mashambulizi yanayohusishwa na Iran.
Katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Dover, Trump alionekana akipiga saluti huku majeneza yaliyobeba miili ya wanajeshi hao yakishushwa kutoka kwenye ndege ya kijeshi.
Waliopotea maisha kwenye uwanja wa mapambano wametambuliwa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani kuwa Tyler James Feehan mwenye umri wa miaka 25 kutoka Hawaii, Isabella Gonzales mwenye umri wa miaka 19 kutoka Texas, Angel S. Rampersad mwenye umri wa miaka 28 kutoka New York, na Michael Emmanuel Swinton mwenye umri wa miaka 30 kutoka North Carolina.
Feehan na Gonzales waliuawa katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran nchini Jordan. Mabaki ya Rampersad, ambaye alikuwa ametoweka kufuatia mashambulizi hayo, pia yalirejeshwa nchini Marekani baada ya kutambuliwa. Swinton naye aliuawa nchini Iraq katika mlipuko uliosababishwa na ndege isiyo na rubani inayohusishwa na Iran.
Tangu kuanza kwa vita mwezi Februari, wanajeshi 18 wa Marekani wameuawa na zaidi ya 450 kujeruhiwa.