Saudi Arabia na Marekani zimesaini makubaliano ya ushirikiano kuhusu matumizi ya nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili katika sekta ya nishati na teknolojia za kisasa.
Makubaliano hayo, yanayojulikana kama “123 Agreement”, yalisainiwa na Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Prince Abdulaziz bin Salman, pamoja na Waziri wa Nishati wa Marekani, Chris Wright. Sambamba na hilo, pande hizo pia zilisaini makubaliano ya ulinzi wa nyenzo za nyuklia (bilateral safeguards agreement).
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati ya Saudi Arabia, makubaliano hayo yanajengwa juu ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Riyadh na Washington, na yanakuja kufuatia tangazo la Mwanamfalme Mohammed bin Salman wakati wa ziara yake nchini Marekani Novemba mwaka jana kuhusu kukamilika kwa mazungumzo ya ushirikiano wa matumizi ya nyuklia kwa amani.
Mkataba huo unalenga kuimarisha ushirikiano katika nyanja za nishati na teknolojia za hali ya juu, kurahisisha kubadilishana utaalamu, maarifa na teknolojia, pamoja na kuhakikisha viwango vya juu vya kimataifa vya usalama wa nyuklia, ulinzi wa nyuklia na kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia.
Akizungumzia hatua hiyo, Waziri wa Nishati wa Marekani, Chris Wright, alisema makubaliano hayo yanaonyesha dhamira ya pamoja ya Marekani na Saudi Arabia ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kukuza ustawi wa kiuchumi ndani ya nchi zao na kuimarisha usalama wa washirika wao duniani.