Umoja wa Afrika (AU) umemteua rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto.
Uteuzi huo umeidhinishwa jijini Addis Ababa kufuatia mapendekezo ya kamati ya Africa CDC, ukitambua mchango na jitihada za Rais Samia katika kuimarisha mifumo ya afya na kukuza maendeleo ya kijamii barani Afrika.
Katika wadhifa huo wa mwaka mmoja, Rais Samia ataongoza juhudi za kuimarisha mshikamano wa nchi wanachama wa AU katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuhamasisha uongozi wa kisiasa katika sekta ya afya.
Lengo kuu la nafasi hiyo ni kuongeza uwekezaji endelevu katika huduma za afya kama sehemu muhimu ya utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Afrika, inayolenga kujenga bara lenye ustawi, afya bora na maendeleo jumuishi.
Aidha, Rais Samia anatarajiwa kuhamasisha ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha ahadi za kimataifa zinatafsiriwa kuwa hatua za vitendo katika ngazi ya kitaifa na kikanda.
Hata hivyo kupitia jukumu hilo pia atakuza mfumo wa kubadilishana uzoefu na mbinu bora miongoni mwa nchi za Afrika, huku Tanzania ikiendelea kuimarisha nafasi yake ya uongozi katika kulinda haki ya kila mwanamke na mtoto kupata huduma bora za afya.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime