Hospitali kubwa na ya mwisho inayofanya kazi huko Gaza- al-Nasser, imelaani uamuzi wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF kusitisha operesheni zake katika ukanda huo kufuatia wasiwasi wa uwepo wa watu wenye silaha.
Hospitali hiyo ilisisitiza kuwa imeimarisha usalama karibu na hospitali hiyo. Msuguano huo wa nadra kati ya taasisi hizo mbili zinazotoa huduma ya afya huko Gaza unashuhudiwa huku idadi ya vifo vya Wapalestina tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano imepindukia sasa watu 600, hii ikiwa ni kutokana na mashambulizi mapya ya Israel.
Hayo yakiarifiwa, Rais wa Marekani Donald Trump amesema hapo jana kuwa nchi zilizoamua kujiunga na Bodi yake ya Amani, zimeahidi kutoa kitita cha dola bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi mpya wa Gaza iliyoharibiwa na vita na kwamba zitachangia maelfu ya wanajeshi katika kikosi cha kimataifa kitakachokuwa na jukumu la ulinzi na usalama katika eneo hilo.