Ikiwa leo ni Siku ya Redio Duniani, wito umetolewa kwa watangazaji na waandishi wa habari kuzingatia uzalishaji wa maudhui bora yenye kuelimisha, kuburudisha na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Wito huo umetolewa na baadhi ya wanahabari walipozungumza na Jembe Habari kuhusu umuhimu wa siku hiyo kwao.
Tonny Alphonce wa BMG Online amesema tasnia ya habari imeendelea kuwa kiungo muhimu katika kuunganisha watu na kuwa chachu ya mabadiliko ya kijamii.
Amehimiza wanahabari kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia zilizopo kwa sasa ili kuongeza ufanisi na ubora wa maudhui.
Kwa upande wake, Sharifat Shinji wa Buha FM ya Kasulu Kigoma amesema wadau wa redio wanafurahia kuona maendeleo ya teknolojia yanavyoendelea kuchukua nafasi kubwa, ikiwemo matumizi ya akili unde (Artificial Intelligence) katika kusaidia uhakiki wa takwimu na upatikanaji wa taarifa za kihistoria.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa redio kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia hiyo ili kuepuka madhara au matumizi mabaya yanayoweza kuathiri jamii.
Itakumbukwa kuwa kila mwaka ifikapo Februari 13 huadhimishwa Siku ya Redio Duniani, ambapo kwa mwaka 2026 kaulimbiu ni “Radio na Akili Unde.”
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime