Rais Samia Atuma Salamu za Pole Kifo cha Mzee Mtei

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mzee Edwin Isaac Mbiliewi Mtei kilichotokea usiku wa kuamkia Januari 19 mwaka huu jijini Arusha.

Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu Rais Dkt. Samia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mzee Mtei, ambaye ni mmoja wa viongozi waliotoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa niaba yake binafsi, Rais Samia ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wote walioguswa na msiba huo mzito.

Rais Samia amemkumbuka Marehemu Mtei kama mtumishi na kiongozi mahiri aliyetoa mchango mkubwa katika sekta ya fedha, mipango na uchumi wa Taifa, akihudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo kuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanzia mwaka 1966 hadi 1974 ambapo alihusika kwa kiasi kikubwa katika kuweka misingi ya uendeshaji wa benki kuu na mfumo wa fedha nchini.

Aidha Rais Samia amesema Mzee Mtei ataendelea kukumbukwa katika historia ya siasa za vyama vingi nchini kama mmoja wa waanzilishi wa demokrasia ya ushindani wa vyama, akiwa miongoni mwa waasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Rais pia ameeleza kuwa mchango wa Marehemu Mtei utaendelea kuenziwa kupitia maandiko yake binafsi, hususan wasifu wa maisha (autobiography), unaoeleza safari yake ya maisha na uongozi katika kulijenga Taifa la Tanzania.

Rais Dkt. Samia ameiombea familia ya marehemu faraja, nguvu na amani katika kipindi hiki kigumu, na kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Edwin Mtei mahali pema peponi.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii