Mvutano wa kisiasa nchini Uganda umeongezeka zaidi baada ya mkuu wa jeshi la nchi hiyo Jenerali Muhoozi Kainerugaba kutoa vitisho vya wazi vya kumuua kiongozi wa upinzani Bobi Wine kufuatia uchaguzi mkuu uliomrejesha madarakani Rais Yoweri Museveni kwa muhula wa nane.
Kainerugaba ambaye ni mwana wa Rais Museveni na pia mkuu wa majeshi ya ulinzi ya Uganda (UPDF) aliandika ujumbe mkali kwenye mtandao wa X akisema kuwa anatamani kumuona Bobi Wine akiwa amekufa ambapo kauli hiyo ilitolewa siku chache baada ya Wine kusema amelazimika kujificha kufuatia uvamizi wa vikosi vya usalama nyumbani kwake.
Aidha vitisho hivyo vilijiri baada ya Museveni mwenye umri wa miaka 81 kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika wiki iliyopita kwa kupata asilimia 71.6 ya kura kwa mujibu wa matokeo rasmi. Ushindi huo umekosolewa vikali na waangalizi wa uchaguzi na mashirika ya haki za binadamu.
Mpinga wake mkuu Bobi Wine—mwanamuziki maarufu aliyebadilika kuwa mwanasiasa mwenye umri wa miaka 43 na jina halisi Robert Kyagulanyi—alitangazwa kuwa wa pili kwa kupata asilimia 24 ya kura kupitia chama chake cha National Unity Platform (NUP).
Katika ujumbe wake wa usiku wa Jumatatu, Kainerugaba aliandika: “Tumeua magaidi 22 wa NUP tangu wiki iliyopita. Ninaomba wa 23 awe Kabobi,” akitumia jina la dharau kumrejelea Bobi Wine Katika chapisho jingine alimpa Wine saa 48 ajisalimishe kwa polisi, akitishia kumchukulia kama mhalifu endapo hatofanya hivyo.
Bobi Wine alilaani kauli hizo akizitaja kuwa vitisho vya moja kwa moja vya kumuua. Alisema majeshi ya usalama yamezingira makazi yake na kuhatarisha usalama wa familia yake Mke wake anadaiwa kuwa chini ya kifungo cha nyumbani, huku alipo Wine mwenyewe bado hakijulikani baada ya kusema alinusurika kwa taabu uvamizi wa kijeshi uliofanyika Jumamosi.
Katika ujumbe wa televisheni uliorushwa Jumatatu usiku kupitia NTV Uganda Wine aliishutumu polisi kwa kuharibu nyumba yake na kusema kuondoka hapo kulimwezesha “kuzungumza na dunia,” bila kuweka wazi alipo.
Kainerugaba anayejulikana kwa kauli zake kali na za uchochezi mitandaoni, aliendelea kuongeza lugha ya matusi akijitaja kuwa “nabii wa Mungu Mwenyezi” na kumtukana Bobi Wine kwa maneno ya kudhalilisha utu. Mwaka jana aliwahi pia kutishia kumkata kichwa kiongozi huyo wa upinzani.
Vitisho vipya vimekuja baada ya kipindi kifupi ambacho Kainerugaba alikuwa kimya wakati wa kampeni lakini alirejea kwa nguvu mitandaoni mara tu baada ya ushindi wa baba yake kutangazwa.
Msako na kukamatwa Wakati huo huo ukandamizaji dhidi ya upinzani umeendelea kushika kasi. Zaidi ya wanachama 118 wa chama cha NUP walifikishwa mahakamani jijini Kampala Jumatatu na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo mkusanyiko haramu, kula njama na kumiliki vifaa vya uchaguzi kinyume cha sheria.
Katibu Mkuu wa NUP, David Rubongoya alikanusha madai kuwa wafuasi wa chama hicho walihusika katika vurugu akisema wengi wa waliokamatwa walikuwa mawakala halali wa uchaguzi.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime