Trump ajaribu ´kutuliza joto´ Minneapolis

Rais Donald Trump wa Marekani amesema amemtuma Afisa Mkuu wa Uhamiaji na Ulinzi wa Mipaka ya nchi hiyo kwenda kusimamia oparesheni za kuwasaka wahamiaji wasio na vibali kwenye mji wa Minneapolis.

Uamuzi huo umetafsiriwa kuwa unalenga kutuliza hasira ya umma baada ya maafisa uhamiaji kumuua mtu wa pili kwenye mojawapo ya oparesheni zao.

Trump ameonesha ishara ya kutafuta suluhu baada video iliyooonesha maafisa uhamiaji wakimpiga risasi na kumuua raia mwingine kuzusha maandamano makubwa ya umma na ukosoaji kutoka kwa marais wa zamani Bill Clinton na Barack Obama.

Trump amesema Tom Homan -- ambaye anaongoza Idara ya Taifa ya Uhamiaji na Mipaka -- atakwenda kusimamia oparesheni zinazoendelea na kwamba amefanya mazungumzo na Gavana wa jimbo la Minnesota uliko mji wa Minneapolis pamoja na meya wa mji huo.

Hatua hizo, zinaashiria mabadiliko ya mtazamo ndani ya utawala Trump kuhusu oparesheni zake za kuwasaka wahamiaji ambazo mara kadhaa zimehusisha matumizi makubwa ya nguvu ya dola.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii