Paul Mackenzie ameshtakiwa kwa kuhusishwa na vifo vipya 52

Nchini Kenya kumekuwa na mabadiliko katika kesi ya kundi la kiimani la Shakahola. Paul Mackenzie, mchungaji aliyejitangaza, atashtakiwa kwa vifo vipya 52. Mchungaji huyo aliyejitangaza yuko kizuizini kabla ya kesi tangu mwaka 2023, kama sehemu ya uchunguzi wa vifo vya takriban wafuasi 450 wa dhehebu lake, ambao aliwahimiza kufunga hadi kufa ili kukutana na Yesu katika msitu wa Shakahola mashariki mwa Kenya. 

Mnamo mwaka 2025, miili 34 na sehemu 102 za miili ziligunduliwa katika kijiji cha Binzaro, takriban kilomita 30 kutoka Shakahola. Kulingana na uchunguzi, Vyote hivi vinalingana na vifo vya watu 52. Wachunguzi wanaelezea mwendelezo wa ibada ya Shakahola hata wakati mchungaji huyo alikuwa kizuizini.

Miongoni mwa washukiwa katika kesi ya Binzaro ni wanachama wa zamani wa kundi hili la kiimani la Shakahola. Katika taarifa yake, upande wa mashtaka unadai kwamba "kuna mashaka yanayofaa kuhusu Paul Mackenzie, anayeshukiwa kuwa na wazo na kusimamia utendakazi wa makosa hayo, akitumia mafundisho yenye msimamo mkali […] kuwavutia waathiriwa wa Binzaro." Wachunguzi wamepata maelezo yaliyoandikwa kwa mkono kutoka huko anakozuiliwa, ambayo yanaripotiwa kuelezea miamala iliyofanywa kupitia simu za mkononi.

Kulingana na vyombo vya habari vya Kenya, wafuasi wanne wanadaiwa kuendelea na shughuli za kundi hilo ili kuwavutia waathiriwa wapya wa Binzaro, chini ya usimamizi wa Paul Mackenzie, ambaye inadaiwa aliendelea na mahubiri yake kwa simu kutoka mahali anakozuiliwa.

Upande wa mashtaka wa Kenya sasa unataka kuchanganya kesi hizo mbili. Paul Mackenzie tayari ameshtakiwa, miongoni mwa mambo mengine, kwa "mauaji, mauaji bila kukusudia, na itikadi kali" katika kesi ya kundi la kiimani la Shakahola. Katika kesi hii mpya, yeye na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka kadhaa, kulingana na upande wa mashtaka, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli za uhalifu zilizopangwa, itikadi kali, kuwezesha vitendo vya kigaidi, na mauaji.

Paul Mackenzie amepangwa kufikishwa mahakamani mnamo Februari 11 kwa ajili ya kusikiliza kesi inayohusiana na kesi hii ya hivi karibuni.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii