Waziri Mkuu Akagua Kituo cha Uokozi Ukanda wa Ziwa Victoria

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (MB) mapema leo  Januari 23 mwaka huu ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kuratibu Ufuatiliaji na Uokozi katika Ukanda wa Ziwa Victoria kilichopo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza na wananchi baada ya ukaguzi huo Dkt. Nchemba amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuthamini maisha ya wananchi kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inalenga kuimarisha usalama hususan kwenye maeneo yenye changamoto za ajali za majini.

Ambapo amesisitiza kuwa kituo hicho kinahusisha masuala ya dharura hivyo amewataka watendaji na wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kuwa makini na kutofanya uzembe huku akionya kuwa kusinzia katika utekelezaji kunaweza kusababisha maafa na kuharibu vifaa vya kisasa vilivyowekezwa kwa gharama kubwa.

“Mradi huu unahusu uokozi wa maisha ya watu"Msipofanya kazi kwa umakini mtaangamiza maisha ya wananchi pamoja na vifaa vya gharama kubwa vilivyowekwa kwa fedha za Serikali na washirika wetu,” amesema Dkt. Nchemba.

Akimkaribisha Waziri Mkuu Waziri wa Uchukuzi Mhe. Profesa Makame Mbarawa amesema Ukanda wa Ziwa Victoria umekuwa na changamoto kubwa ya ajali za majini ambapo takribani watu 20 wamepoteza maisha katika kipindi cha hivi karibuni hali iliyoisukuma Serikali kuanzisha kituo hicho cha uokozi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mohamed Salum amesema kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kimataifa wa Afrika Mashariki wa kuzuia ajali na upotevu wa maisha majini uliopitishwa na Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki mwaka 2007.

Ameongeza kuwa kati ya mwaka 2022 hadi 2025 Tanzania na Uganda zilianza utekelezaji wa pamoja wa mradi huo kwa lengo la kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri majini na shughuli za uvuvi kupitia mifumo ya ufuatiliaji wa kisasa.

Amesema kwa upande wa Tanzania mradi huo unagharimu shilingi bilioni 19.8 ukiwahusisha ujenzi wa vituo vitatu vya uokozi, ununuzi wa boti, maboya, pamoja na jengo la kituo kikuu cha ufuatiliaji na taarifa za hali ya hewa.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii