Bobi Wine Akataa Matokeo ya Uchaguzi Uganda

Wiki moja baada ya uchaguzi wa urais nchini Uganda ambao Rais Yoweri Museveni alitangazwa kuwa mshindi ambapo  kiongozi wa upinzani Bobi Wine amesema hatambui matokeo hayo huku akidai yaligubikwa na udanganyifu na ukandamizaji akizungumza navyombo mbalimbali vya habari Bobi Wine alisema yuko mafichoni kwa hofu ya usalama wake.

Sambamba na hayo  Bobi Wine alieleza kuwa  anawindwa na vyombo vya usalama licha ya kutuhumiwa au kushtakiwa kwa kosa lolote aliongeza kuwa familia yake imezingirwa na wanajeshi na haiwezi kuondoka wala kupokea misaada ya chakula.

Kiongozi huyo wa upinzani amedai kuwa raia wamekuwa wakipigwa risasi na kuuawa katika maeneo mbalimbali ya nchi tangu uchaguzi wa Januari 15.

Amedai kuwa zaidi ya watu 100 wameuawa, huku wengine wakikamatwa bila kufuata taratibu za kisheria.

Bobi Wine amesema baadhi ya manaibu na wasaidizi wake wamekamatwa, wakiwemo wanawake wawili waliokamatwa siku moja kabla ya uchaguzi na ambao bado hawajulikani walipo pia amedai kuwa naibu wake wa eneo la kati alikamatwa siku ya Alhamisi.

Vilevile akizungumzia tukio la Butambala Bobi Wine amedai kuwa wafuasi wake kumi waliuawa siku ya uchaguzi nyumbani kwa mbunge Muhammad Muwanga Kivumbi.

Kwa mujibu wa Bobi Wine, wanane kati ya waliouawa walikuwa wanawake waliokuwa wakihifadhi fomu za matokeo ya vituo vya kupigia kura.

Na katika mada ya udanganyifu wa uchaguzi Bobi Wine amesema kwamba upinzani una ushahidi unaodai kuonyesha udanganyifu wa kabla, wakati na baada ya upigaji kura, ikiwemo video za maafisa wa usalama na wa Tume ya Uchaguzi wakijaza kura.

Amedai kuwa matokeo yalitangazwa bila kuchapishwa fomu za matokeo kutoka vituo vya kupigia kura.

Hivyo kiongozi huyo wa upinzani amesema hatatafuta suluhu ya kisheria, akidai hana imani na uhuru wa mahakama nchini Uganda ambapo amesema kuwa matumaini ya upinzani yako kwa wananchi kusimama na kupinga kile alichokitaja kuwa matokeo yasiyo halali.

Aidha ametoa wito kwa raia wa Uganda kuendesha maandamano yasiyo na vurugu na kuchukua hatua za amani kupinga serikali.

Amesema harakati hizo hazihusiani na uchaguzi wa baadaye bali kurejesha demokrasia.

Hata hivyo Bobi Wine ameitaka jumuiya ya kimataifa kuichukulia serikali ya Uganda kwa misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.

Amesisitiza kuwa Afrika inapaswa kutendewa kwa viwango sawa na kanda nyingine za dunia.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii