Waziri Mkuu Aagiza Mradi wa Maji Mwanza Ukamilike Haraka

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Januari 23 mwaka huu ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha kusukuma maji na matenki ya kuhifadhia maji unaotekelezwa Mtaa wa Sahwa, Kata ya Lwanhima, Jijini Mwanza.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Nchemba amewataka wakandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa haraka kwa lengo la kuondoa kero ya maji kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa Serikali itakuwa makini katika kuusimamia utekelezaji wake.

Aidha, amemuagiza Waziri wa Maji kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maji zinafika kwenye miradi kwa wakati, akibainisha kuwa maji ni huduma ya kijamii isiyo na mbadala kwa ustawi wa wananchi.

Akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (MB) amesema wizara yake kwa kushirikiana na Katibu Mkuu watahakikisha wanamsimamia mkandarasi kikamilifu ili mradi ukamilike kwa muda uliopangwa kwenye mkataba.

Awali, akisoma taarifa ya mradi, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Nelly Msuya, amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi SINOHYDRO Corporation Limited & Highland Build Co., Ltd (JV) na ni sehemu ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Ziwa Victoria (LVWATSAN).

Ameeleza kuwa mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji wa majisafi na huduma za usafi wa mazingira kwa Jiji la Mwanza na maeneo jirani, na unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wakazi 450,000 wa Mwanza, Magu na Misungwi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Nyegezi, Buhongwa, Igoma, Kisesa, Bujora na Usagara.

Mradi huo ulianza kutekelezwa Juni 2024 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 46, hatua itakayochangia kupunguza magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo salama.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii