Maambukizi ya damu yanayosababishwa na vimelea zaidi ya mmoja yanaendelea kuwa changamoto kubwa katika hospitali za rufani nchini Tanzania, huku yakiongeza hatari ya vifo, hususan kwa watoto wachanga.
Hayo yamebainishwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kupitia matokeo ya utafiti wake uliopewa jina “Outcomes of the First Stem Cell Transplant Program in Tanzania, East Africa”, uliochapishwa katika jarida la MNH Research Abstract Book: From Data to Impact.
Kwa mujibu wa utafiti huo, uliotumia takwimu za wagonjwa waliolazwa kati ya Julai 2021 na Juni 2022, wagonjwa waliokuwa na maambukizi ya damu yanayosababishwa na vimelea zaidi ya mmoja walionesha matokeo mabaya zaidi ya kiafya ikilinganishwa na wale walioambukizwa na kimelea mmoja pekee.
Utafiti huo ulihusisha wagonjwa 200, wakiwamo wagonjwa 50 waliokuwa na maambukizi ya vimelea zaidi ya mmoja na wagonjwa 150 waliokuwa na maambukizi ya kimelea mmoja.
Watafiti walieleza kuwa makundi hayo mawili hayakuonesha tofauti kubwa katika vigezo vya kijinsia wala uwepo wa magonjwa mengine ya awali, hali iliyowawezesha kuchambua moja kwa moja athari zinazotokana na aina ya maambukizi ya damu.
Matokeo yalionesha kuwa katika maambukizi ya vimelea zaidi ya mmoja, bakteria kama Klebsiella pneumoniae na Enterobacter walionekana mara nyingi, huku katika maambukizi ya kimelea mmoja bakteria waliotawala wakiwa ni Staphylococcus aureus, Klebsiella pneumoniae na Acinetobacter.
Utafiti huo umeonesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya uchunguzi wa maambukizi ya damu pamoja na matumizi sahihi ya dawa za kuua vimelea, ili kupunguza vifo na madhara kwa wagonjwa, hususan watoto wachanga katika hospitali za rufani.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime