EC Uganda Yapiga Marufuku Bendera ya Taifa Katika Vituo vya Kupiga Kura

Tume Huru ya Uchaguzi ya Uganda (EC) imepiga marufuku wapigakura kubeba au kupeperusha Bendera ya Taifa katika vituo vya kupiga kura, ikionya dhidi ya matumizi ya nembo za taifa kwa malengo ya kisiasa wakati wa zoezi la uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Simon Byabakama wa Mahakama ya Rufani ya Uganda, alisema kuwa Bendera ya Taifa ni mali ya wananchi wote na haipaswi kutumika kama nyenzo ya kampeni za kisiasa.

“Bendera ya Taifa ni ya Waganda wote. Sio nyenzo ya kampeni na haipaswi kuletwa katika vituo vya kupiga kura,” alisema Byabakama.

Alifafanua kuwa matumizi ya Bendera ya Taifa yanadhibitiwa na sheria, ambayo inapiga marufuku matumizi ya nembo za taifa kwa madhumuni ya kisiasa au kibiashara bila kibali maalum kutoka Wizara ya Sheria na Masuala ya Katiba.

Mbali na marufuku hiyo, Tume ya Uchaguzi pia imekataza wapigakura kuvaa tisheti zenye nembo za vyama vya siasa, kubeba picha za wagombea au kuonyesha rangi za vyama vyao katika vituo vya kupiga kura.

Kwa mujibu wa Byabakama, vituo vya kupiga kura vinapaswa kubaki huru na visivyoegemea upande wowote ili kuhakikisha haki, amani na uwazi wa zoezi la uchaguzi.

“Tunawahimiza wapigakura kuacha nyumbani nyenzo zote zinazohusishwa na vyama vya siasa au picha za wagombea kabla ya kufika vituoni,” alisisitiza.

Hatua hiyo imekuja wakati ambapo kiongozi wa upinzani nchini humo, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amekuwa akiwahamasisha wafuasi wake kubeba Bendera ya Taifa wakati wa kampeni kama ishara ya utaifa.

Hata hivyo raia wa Uganda wanatarajiwa kupiga kura Januari 15, 2026, kuwachagua viongozi watakaohudumu katika muhula ujao wa uongozi wa nchi hiyo.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii