Wafanyabiashara sita wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi inayohusisha kuwasilisha nyaraka za uongo katika Bandari ya Dar es Salaam na kujipatia zaidi ya Sh10 bilioni kutokana na shehena ya mafuta leo Jumanne Januari 13, 2026 wanatarajiwa kusomewa maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo vya upande wa Jamhuri.
Hatua hiyo inakuja baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika ambapo upande wa mashtaka umeeleza kuwa uko tayari kuanza kuwasilisha ushahidi wake mahakamani.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Joseph Matage, Grace Matage ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya RHG General Traders Ltd na pia wakala wa forodha Jamaal Saad, Mubinkhan Dalwai, Stanley Tibihenda na Edward Omeno, wote wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambapo kesi hiyo yenye namba 5195 ya mwaka 2025, inasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 13 yakiwamo ya kula njama kuwasilisha nyaraka za uongo katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na kujipatia kiasi cha zaidi ya Sh10 bilioni kilichotokana na shehena ya mafuta.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime