Kesi ya wagombea wa ACT Pemba yaahirishwa hadi Desemba 23

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Kanda ya Pemba, Chausiku Kuya, ameahirisha kesi ya madai iliyofunguliwa na waliokuwa wagombea wanane wa Uwakilishi kupitia chama cha ACT Wazalendo Kisiwani Pemba hadi Desemba 23, 2025.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya mawakili wa upande wa wadai kuiomba Mahakama iwape muda wa siku saba ili kupitia majibu ya maandishi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi, pamoja na kuandaa majibu ya kinzani kwa kina na kwa kuzingatia taratibu za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, Wakili Omar Said Shaaban, ambaye pia ni kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai, alisema kuwa ombi la kupewa muda lililenga kuhakikisha hoja zote za utetezi zinajibiwa kwa usahihi na kwa kufuata misingi ya sheria.

“Tunapewa muda wa siku saba kuandaa majibu yetu. Ikifika tarehe hiyo, kila kitu kitakuwa kimekamilika, kisha Naibu Msajili atayawasilisha mafaili yote kwa Jaji Mkuu kwa ajili ya kupanga majaji watakaosikiliza kesi hizi,” alisema Wakili Shaaban.

Aliongeza kuwa upande wa wadai umeridhika na hatua hiyo ya Mahakama na kwamba maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea hatua zinazofuata za mashauri hayo.

Wakili Shaaban aliwataka waliokuwa wagombea waliowasilisha madai hayo pamoja na wafuasi wa chama cha ACT Wazalendo kuwa watulivu na wenye subira wakati kesi hizo zinaendelea Mahakamani.

“Sisi kama mawakili wenu tunawahakikishia kuwa haki itazingatiwa na kila hatua itafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu zote za kisheria,” alisisitiza.

Kwa upande wa Serikali, kesi hiyo inawakilishwa na jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Mbarouk Suleiman Othman kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Majimbo yanayolalamikiwa katika mashauri hayo ni Kiwani, Mkoani, Chakechake, Chonga, Wawi, Kojani, Konde na Micheweni.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii