Mahakama yaamua PSG imlipe Mbappé zaidi ya dola milioni 70

Mahakama ya Paris inayohusika na masuala ya ajira imeamua kwamba Paris Saint-Germain lazima imlipe Kylian Mbappé zaidi ya euro milioni 60 (dola milioni 70).

Ni kuhusu mzozo wa mshahara na bonasi ambazo hazijalipwa zinazohusiana na kumalizika kwa mkataba wake kabla ya kuhamia Real Madrid mwaka wa 2024.

Mawakili walitoa hoja zao mahakamani mwezi wa Novemba katika sakata la kisheria lililohusisha kiasi kikubwa cha pesa. Mahakama siku ya Jumanne ilimuunga mkono mchezaji huyo huku kukiwa na shutuma za usaliti na unyanyasaji unaozunguka kuvunjika kwa uhusiano wake na PSG.

Mawakili wa Mbappé walisema kuwa anaidai PSG zaidi ya euro milioni 260 (dola milioni 305), nayo PSG ilikuwa ikimtaka Mbappé aipe euro milioni 440, kama fidia na "kupoteza fursa" baada ya kuondoka kwa uhamisho huru.

Uamuzi huo wa mahakama unaweza kukatiwa rufaa na hakuna uwezekano wa kuumaliza mzozo huo.

Mawakili wa Mbappé walisema uamuzi huo "unathibitisha kwamba mikataba lazima iheshimiwe. Unarejesha ukweli rahisi: Hata katika sekta ya mpira wa miguu sheria za kazi zinatumika kwa kila mtu."

Hakujatolewa kauli ya haraka kutoka kwa PSG.

Uhusiano kati ya mshindi huyo wa Kombe la Dunia la 2018 na bingwa huyo mtetezi wa Ulaya uligeuka kuwa mchungu wakati Mbappé alipoamua mwaka wa 2023 kutourefusha mkataba wake, ambao ulipangwa kuisha katika msimu wa joto wa 2024.

Hii iliinyima klabu fursa ya kufanya uhamisho wenye kiasi kikubwa cha fedha licha ya kumpa mkataba mzuri zaidi katika historia ya klabu hiyo aliposaini mkataba mpya mwaka wa 2022.

Aliondolewa kwenye ziara ya maandalizi ya msimu na kulazimika kufanya mazoezi na wachezaji wa pembeni. Alikosa mchezo wa ufunguzi wa ligi lakini akarudi kwenye kikosi kwa msimu wake wa mwishobaada ya majadiliano na klabu - mazungumzo ambayo ndicho kiini cha mzozo huo wa mahakamani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii