Polisi wapiga risasi washukiwa waliowakuta wakipora maduka usiku

WASHUKIWA wawili wa wizi wanauguza majeraha ya risasi baada ya polisi kutibua njama zao eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa.

Walikuwa kwenye kundi la wezi waliokuwa wakipora duka usiku wa kuamkia jana.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa tisa na dakika ishirini asubuhi katika duka lililoko eneo la Shonda.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, maafisa waliokuwa wakishika doria walipokea wito wa dharura kutoka kwa mmiliki wa duka hilo, aliyeripoti kuwa watu wasiojulikana walikuwa wakivamia biashara yake.

Polisi walisema walipofika eneo la tukio, walikuta karibu watu wanane waliokuwa wamejihami kwa silaha hatari wakiendeleza uporaji huo.

“Washukiwa hao walitoroka walipowaona maafisa wa polisi, hali iliyowalazimu polisi kufyatua risasi walipokuwa wakiwafuatilia,” ripoti ya polisi ilieleza.

Mshukiwa mmoja alikamatwa katika eneo la tukio. Katika harakati za kuwasaka washukiwa waliotoroka, polisi waliwakuta wengine wawili wakiwa wamelala barabarani bila fahamu kutokana na majeraha ya risasi.

Mmoja alipata jeraha la risasi kwenye mguu wa kushoto chini ya goti, na mwingine alipigwa risasi kwenye ubavu wake wa kushoto.

Polisi waliwapata na simu tatu za mkononi, ambapo simu mbili zilitambuliwa kikamilifu na mlalamishi kuwa ni mali iliyokuwa imeibwa kutoka dukani mwake.

Silaha na vifaa kadhaa vinavyoaminika kutumika katika wizi huo pia vilipatikana katika eneo la tukio. Vifaa hivyo ni pamoja na panga, vyuma na rungu moja.

Aidha, polisi walipata pikipiki tatu zinazodhaniwa kutumiwa na genge hilo kutoroka baada ya tukio.

Wakati wa shambulio hilo, mlinzi wa duka hilo, alijeruhiwa kidogo baada ya kushambuliwa kwa kifaa butu na genge hilo kabla ya kuvunjwa kwa duka.

“Washukiwa wote, pamoja na vielelezo vilivyopatikana, walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Inuka huku wakisubiri hatua zaidi za kisheria,” taarifa ya polisi ikasema.

Washukiwa wawili waliojeruhiwa pamoja na mlinzi huyo walipelekwa Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Likoni kwa matibabu.

“Mlinzi alitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani akiwa katika hali nzuri na thabiti, huku washukiwa waliojeruhiwa wakiendelea kupokea matibabu chini ya ulinzi mkali wa polisi,” ikaongeza.

Polisi wamesema kuwa bado wanwasaka washukiwa wengine waliotoroka huku wakiendelea na uchunguzi zaidi.

Kisa hicho kimetokea wakati ambapo polisi wamezidisha doria katika sehemu mbalimbali za Kaunti ya Mombasa, ili kuepusha visa vya uhalifu wakati wa shughuli nyingi za msimu wa likizo.

Hivi majuzi, Kamanda wa Polisi Mombasa Peter Kimani, alisema maafisa wa polisi wamewekwa katika maeneo yanayotembelewa na watu wengi wakati wa likizo, ikiwemo Pembe za Ndovu, Mwembe Tayari na bustani ya Mama Ngina.

Vilevile, doria zimezidishwa katika mitaa ambayo hushuhudia uhalifu wa mara kwa mara kutoka kwa magenge ya vijana ikiwemo Likoni, Kisauni, Nyali na sehemu za Mvita kama vile Old Town.

“Tumekamilisha ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuhakikisha watalii na wakazi wanahisi salama,” alisema Bw Kimani.

Aliongeza kuwa, polisi pia watapiga doria katika ufukwe maarufu wa Shelly, Jomo Kenyatta na Nyali ili kuhakikisha hakuna matukio ya uhalifu au ajali.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii