Ng’ombe 22 wa mfugaji Alex Idege, mkazi wa Kijiji cha Kasingili, Kata ya Ilola, Wilaya ya Shinyanga, wamekutwa wamekufa zizini muda mfupi baada ya kurejea kutoka malishoni, katika tukio linaloibua maswali mengi juu ya chanzo cha vifo hivyo.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Idege amesema kuwa saa 10 alfajiri alisikia ng’ombe wake wakilia, hali iliyomfanya atoke nje na kuamulika zizini ambapo aliwaona wakiwa salama, ndipo akarudi kulala.
Hata hivyo, saa 11 asubuhi, kijana aliyefika kwa ajili ya kufunga ng’ombe kwenda shambani aligundua kuwa mifugo hiyo ilikuwa imekufa na kumpa taarifa mara moja.
Idege amesema alipofika zizini alikuta ng’ombe sita tayari wamekufa na wengine wakiwa katika hali mbaya, lakini kadri muda ulivyopita waliendelea kufa hadi kufikia ng’ombe 22, huku wakisalia ndama watatu pekee ambao hawakupelekwa malishoni siku hiyo.
Ameeleza kuwa mifugo yake huwa inalishwa eneo moja kwa muda mrefu bila matatizo, na kusema kuwa maelezo ya awali kutoka kwa mtaalamu wa mifugo kuwa huenda walikula majani yenye sumu hayamridhishi, akisisitiza kuwa amepata hasara kubwa baada ya kupoteza ng’ombe wake wote 22.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ilola, Kisena Fred, amesema amesikitishwa na tukio hilo na kuomba uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo.
Ameongeza kuwa endapo itabainika kuwa ni ugonjwa, hatua za haraka zichukuliwe ili kuzuia kuenea kwa mifugo ya wananchi wengine.
Naye Ofisa Mifugo wa Kata ya Ilola, Daniel Jilala, amesema kuwa tayari sampuli za mifugo hiyo zimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Ameeleza kuwa ingawa uchunguzi bado unaendelea, matokeo ya awali yanaashiria uwezekano wa mifugo hiyo kula majani yenye sumu.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime