Pwani wajipanga kuwafikia wasio na uwezo kupitia Bima ya Afya kwa Wote

Katika tathmini ya utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Pwani umejipanga kufanya uhakiki wa wananchi wasio na uwezo ili waweze kufikiwa na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.

Hayo yameelezwa mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha tathmini ya utekelezaji wa ahadi hizo.

Kunenge amesema kikao hicho, kilichowakutanisha viongozi mbalimbali kutoka wilaya zote za mkoa huo, kilifikia makubaliano ya kufanya uhakiki wa wananchi wasiokuwa na uwezo ili kuhakikisha kila mmoja ananufaika na huduma ya bima ya afya.

Ameongeza kuwa mkoa unaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu katika sekta zote ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kumsaidia Rais katika kutimiza ahadi zake.

“Eneo tunalohitaji kuongeza nguvu zaidi ni sekta ya afya, hususan kwa wananchi wasio na uwezo wa kumudu bima ya afya. Hili ni eneo tunaloendelea kulifanyia kazi,” amesema Kunenge.

Aidha, amesema kuwa ili kufanikisha mpango huo, taasisi zote za mkoa zinapaswa kuhakikisha mifumo yao inashabihiana na kufanya kazi kwa ushirikiano, ambapo kila taasisi imuone mwenzake kama mteja wake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasr, amesema wilaya hiyo imejenga jengo la Kituo cha Huduma Wezeshi (One Stop Centre) ambacho kitaziwezesha taasisi mbalimbali kuwa na ofisi mahali pamoja kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi kwa urahisi.

Ameeleza pia kuwa katika kipindi cha siku 100 za Rais, Wilaya ya Mkuranga imetenga maeneo matano ya kongani za viwanda, huku viwanda 16 tayari vikiunganishiwa nishati ya gesi, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa umeme.

Naye Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Mawazo Nicas, amesema manispaa hiyo imejipanga kuhakikisha inapata matokeo chanya katika utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii