Papa Leo Asema Matumizi ya Dini Kuanzisha Vita ni Kufuru na Dhambi Kubwa

Papa Leo ambaye ni  kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani leo Vatican City, Desemba 18 mwaka huu amekemea vikali matumizi ya dini kama chombo cha kuhalalisha migogoro ya kisiasa, vurugu, na vita huku akisema kwamba ni kitendo cha kufuru na dhambi kubwa inayomkosea heshima Mungu.

Katika ujumbe wake wa kila mwaka kuelekea Siku ya Amani Duniani, ambayo itafanyika Januari 1, 2026, Papa Leo alitoa wito kwa waumini wote kupinga matumizi mabaya ya dini katika siasa huku akisisitiza kuwa kumtumia Mungu au imani za kidini kuhalalisha vurugu na mapambano ya silaha ni jambo lisilokubalika.

"Kwa bahati mbaya, imekuwa kawaida kuona lugha ya imani ikiburuzwa katika mapambano ya kisiasa, kubariki utaifa, na kuhalalisha vurugu kwa jina la dini," alisema Papa Leo katika ujumbe wake.

Hali ya Vurugu na Kutumia Dini kwa Madhumuni ya Kisiasa

Papa Leo alielezea wasiwasi wake kuhusu baadhi ya viongozi wa dini, ambao amedai wanachochea chuki kwa waumini wao kwa kutumia imani kama daraja la kufanikisha malengo ya kisiasa na kitaifa ambapo aliwaambia waumini kwamba wanapaswa kupinga mwenendo huu kwa vitendo na kwa maisha yao ya kila siku.

"Waumini lazima wapinge kikamilifu, hasa kwa ushuhuda wa maisha yao, aina hizi za kufuru zinazolivunjia heshima jina takatifu la Mungu," alisema.

Papa Leo alisisitiza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuwa waangalifu na kutumika kwa imani zao kwa njia inayoheshimu utu wa kila mtu, badala ya kuhamasisha ghasia.

Ongezeko la Matumizi ya Kijeshi Duniani

Katika ujumbe wake Papa Leo pia alizungumzia ongezeko la matumizi ya kijeshi duniani, akitaja takwimu za Taasisi ya Stockholm ya Utafiti wa Amani (SIPRI), ambazo zinaonyesha kuwa matumizi ya kijeshi yaliongezeka kwa asilimia 9.4 mwaka 2024, na kufikia jumla ya Dola za Marekani trilioni 2.7.

Hali hii inaashiria kuwa dunia inaendelea kuwekeza rasilimali nyingi katika silaha badala ya kutafuta njia za amani. Papa Leo alionya kuwa hii ni hatari kwa usalama na ustawi wa dunia, na kuhimiza viongozi wa dunia kutafuta suluhu za amani badala ya matumizi ya nguvu.

Wito wa Amani Duniani

Katika ziara yake ya kwanza kama Papa mwezi Novemba mwaka huu alienda nchini  Uturuki, ambapo alikutana na viongozi wa Kikristo Mashariki ya Kati. Aliwaambia kuwa lazima wakatae kwa nguvu matumizi ya dini kuhalalisha vita, vurugu, na misimamo mikali pia alisisitiza kuwa amani inapaswa kuwa lengo kuu la maisha ya kidini na kisiasa.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii