Nchini Uganda, usiku wa Jumapili ya wiki iliopita kulifanyika mdahalo wa kwanza wa televisheni kwa nafasi ya Urais, mdahalo ambao kwa mara ya kwanza mgombea wa chama tawala NRM, Yoweri Museveni hakuhudhuria.
Kwa mujibu wa timu ya Kampeni ya rais Museveni, wamekiri kupokea mualiko wa kituo cha NTV Uganda siku 10 kabla ya mdahalo wenyewe, lakini imesema kiongozi wao asingeweza kuhudhuria kutokana na majukumu mengine ya kampeni.
Wagombea wengine wawili Robert Kasibante wa NPP na Mubarak Munyagwa wa CMP pia hawakuhudhuria.
Hata hivyo kinara wa upinzani Robert Kyagulani maarufu kama Bob Wine, alihudhuria mdahalo huo ambapo alishamnbulia rekodi ya miaka 40 ya rais Museveni, akisema hana jipya na wakati umefika wa sura mpya kwenye uongozi.
Aidha agenda kuhusu hali mbaya ya uchumi, ukosefu wa ajira zilitawala mdahalo huo, ambapo wagombea Nathan Nandala Mafabi wa FDC na Frank Bulira Kabinga wa RPP waliahidi kubadili mambo ikiwa watachaguliwa.
Ahadi kama hizo zilitolewa pia na wagombea, Mugisha Muntu wa muungano wa ANT na Joseph Mabirizi wa chama cha Conservative.
Uchaguzi mkuu wa Uganda, umepangwa kufanyika Januari 15 mwakani.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime