ripoti "Sita kati ya watoto 10 duniani hawawezi kusoma licha ya kuwa shuleni,"

WATOTO sita miongoni mwa 10 duniani kote hawajui kusoma sentensi rahisi wala kusuluhisha maswali ya kimsingi ya hesabu licha ya thuluthi yao kuwa shuleni kwa sasa.

Haya ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na shirika linalofahamika kama People’s Action for Learning (PAL) Network iliyotathmini matokeo ya masomo miongoni mwa watoto 89,870 wenye umri wa miaka mitano hadi 16 katika mataifa 12.

Matokeo hayo yamezua wasiwasi mkubwa kuhusu ubora wa elimu katika mataifa mengi maskini kwa kufichua kwamba kuhudhuria shule pekee sio hakikisho la masomo halisi.

Ripoti hiyo inaashiria kwamba Kenya inaongoza majirani zake barani Afrika Mashariki katika kufanikisha Viwango vya Chini zaidi vya Ufaafu (MPL) katika hisabati, licha ya changamoto zinazoendelea kama vile upungufu wa walimu, uhaba wa vifaa vya masomo na maswala yanayohusu vipimo.

Kulingana na ripoti, asilimia 43 ya watoto wenye umri wa miaka 10 nchini wanatimiza kiwango kinachohitajika cha MPL ikilinganishwa na asilimia 33 Tanzania na asilimia 4 Uganda.

MPL ni vipimo maalum vya kimataifa vinavyoonyesha kile ambacho mtoto anahitajika kujua mwishoni mwa elimu ya msingi ya chini.

Vinajumuisha uelewa wa kimsingi wa kusoma na ujuzi wa kimsingi kuhusu tarakimu kama vile kutatua tarakimu kamilifu hadi 100 na kusuluhisha hesabu rahisi.

Matokeo bora kwa kiasi fulani ya Kenya yanaashiria kupiga hatua katika elimu ya kimsingi, ingawa taifa hili bado linavuta mkia ikilinganishwa na nchi zilizoandikisha matokeo bora kama vile Mexico, Nicaragua, na Pakistan.

“Pana haja ya kutathmini upya vifaa vya ufundishaji katika shule zetu kuhakikisha vinapiga jeki somo la tarakimu katika madarasa yetu,” alisema mkurugenzi wa Wizara ya Elimu, Martin Kungania, ripoti za kimataifa kuhusu mitihani ya kimsingi kwa tarakimu (ICAN) na kusoma (ICAR) zilipotolewa.

Udadisi huu uliofanyika wiki ya kwanza ya Januari na wiki ya pili ya Agosti nchini Kenya, ulishirikisha watoto 6,669 na familia 4,459.

Nchi zilizoshiriki udadisi huo ni pamoja na Kenya, Tanzania, Uganda, Senegal, Mali, Mozambique, Botswana, Bangladesh, Pakistan, Nepal, Mexico, na Nicaragua.

Katika sehemu kubwa ya nchi zilizoshiriki, watoto wapatao tisa miongoni mwa 10 wamejiunga na shule, huku wengi wao wakihudhuria taasisi za umma, japo idadi kubwa wanasomea shule za kibinafsi.

Kenya imejitokeza kuwa yenye idadi ndogo zaidi ya watoto wasioenda shule.Hii inaashiria kuwa juhudi za serikali za kufanikisha asilimia 100 ya watoto wanaojiunga na sekondari kutoka shule ya msingi, zinazaa matunda.

Miongoni mwa watoto Wakenya wenye umri kati ya miaka 10 – 14, zaidi ya asilimia 80 wanahudhuria shule za umma, huku asilimia 16 wakihudhuria shule za kibinafsi na kuacha chini ya asilimia mbili ambao hawako shule.

Duniani kote, Mexico inaongoza kwa idadi kubwa zaidi ya watoto waliojiunga na shule za umma kwa asilimia 90 ikifuatiwa na Tanzania asilimia 87 na Mozambique asilimia 85.
#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii