Mkutano mkuu wa 7 wa nchi na Serikali wa umoja wa Afrika na umoja wa Ulaya wahitimishwa jijini Luanda

Mkutano wa 7 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Ulaya (EU) umekamilika jijini Luanda, Angola, baada ya siku mbili za majadiliano ya kina kuhusu mustakabali wa ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya.  

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo uliongozwa na Makamu wa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi. 

Mkutano huo ambao umefanyika kuanzia tarehe 24 hadi 25 Novemba mwaka huu ulijikita katika agenda za  kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika nyanja za amani, usalama, utawala bora, maendeleo ya kiuchumi, ustawi na maendeleo endelevu na umuhimu wa kuongeza utashi katika masuala ya kimataifa.

Wakati wa mkutano huo, viongozi wa AU na EU wamekubaliana kusimamia kwa pamoja juhudi za kudumisha amani na kutatua migogoro, sambamba na kuimarisha taasisi zinazohusika na usalama barani Afrika.

Viongozi wameweka msisitizo katika utawala bora na majadiliano ya kidiplomasia, yakitambua umuhimu wa ushirikiano unaozingatia heshima na maslahi ya pande zote mbili. 

Kwa upande wa uhamiaji na uhamaji, mkutano umeidhinisha kuendelea kujenga mifumo jumuishi na endelevu itakayowezesha uhamaji salama na wa kisheria, huku ukizingatia mahitaji ya kijamii na kiuchumi ya nchi zote husika.

Mkutano pia umeangazia kwa upana suala la kukuza uchumi wa Afrika kupitia maendeleo ya viwanda, kuongezwa kwa thamani ya bidhaa za ndani, na kuimarishwa kwa mauzo ya nje.

Viongozi wa pande zote mbili wamekubaliana kuendeleza jitihada za utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) ili kuongeza ushindani na uharakishaji wa ukuaji wa masoko ya kikanda.

Kwa kuzingatia rasilimali asilia za Afrika, mkutano umejadili umuhimu wa kuimarisha minyororo ya thamani, hususan katika uongezaji thamani wa madini muhimu na adimu yanayohitajika katika viwanda vya kimataifa.

Katika hilo, EU imeonesha nia ya kushirikiana na Afrika kujenga uwezo wa viwanda vya ndani na kuongeza ushiriki wa bara hilo katika minyororo ya thamani ya kimataifa.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii