IEBC"Wala msiwe na hofu, tumejipanga kisawasawa kwa hizi chaguzi ndogo "

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza kuwa ipo tayari kwa uchaguzi mdogo utakaofanyika Alhamisi katika maeneo 24 ya uchaguzi — viti sita vya bunge, kiti kimoja cha Seneti, na viti 17 vya udiwani kote nchini.

Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Marjan Hussein, alihakikishia taifa kuwa tume iko tayari kufanya uchaguzi wa uwazi na haki.

“Wafanyakazi wote wa kusimamia kura wamefunzwa na vifaa vya uchaguzi tayari vimefikishwa katika maeneo ya uchaguzi,” alisema Bw Marjan katika Shule ya Wasichana St Bhakita Siakago, Mbeere Kaskazini, Kaunti ya Embu.

Aliongeza kuwa kazi pekee iliyosalia ni kusambaza vifaa vya kupigia kura kwenye vituo, mchakato ambao unaanza leo Jumatano wakati tume itakapo fungua makasha yaliyofungwa katika vituo vya kuhesabu kura vya kaunti.

Bw Marjan pia alionyesha imani na mpangilio wa usalama.
“Tuna maafisa wa polisi wawili katika kila kituo cha kupigia kura, huku vikosi vya ziada vikizunguka maeneo ya uchaguzi. Hakuna tunachobahatisha,” alisema.

Akizungumzia taarifa za vurugu zinazoweza kutokea Mbeere Kaskazini, Bw Marjan alisema mbinu za kutosha za usalama zimewekwa kufuatia mkutano na vikosi vya usalama vya eneo hilo.
“Waangalizi pia watakuwepo. Hakuna cha kuogopa,” alisema.

Afisa Mkuu wa uchaguzi Mbeere Kaskazini, John Kinyua, alisema tume imebaini maeneo yenye changamoto, hasa yenye milima kama vile Muminji na Evrore, na imehakikisha magari yenye nguvu yatatumiwa ili kuhakikisha vifaa vinafika, hasa wakati wa mvua.

Kwa upande wa Banisa, Kaunti ya Mandera, Kamishna wa IEBC Hassan Noor Hassan aliwaonya maafisa dhidi ya ushiriki katika udanganyifu wowote wa uchaguzi.

“Yeyote atakayepatikana akijihusisha na udanganyifu atabadilishwa na kushitakiwa kisheria,” alisema, akieleza kuwa eneo hilo lina historia ya makosa ya uchaguzi mwaka 2017 na 2022.
“Tuna vifaa vyote na magari tayari kwa Alhamisi,” aliongeza.

Katika Kaunti ya Baringo, ambapo uchaguzi mdogo wa kiti cha Seneti unafanyika kufuatia kifo cha Seneta William Cheptumo Februari 15, Afisa Mkuu wa Uchaguzi  John Mwangi pia alithibitisha maandalizi yamekamilika.
Alisema kuwa makarani wa kura, wakuu wa vituo na naibu wao wamekamilisha mafunzo.

“Vifaa vyote vya uchaguzi vimefikishwa kwenye maghala ya kaunti na vitasambazwa kwenye vituo 1,029 vya kupigia kura Jumatano,” alisema.

Maandalizi yamefanywa katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko katika Baringo Kusini, huku wananchi wakitumia vituo mbadala vya kupigia kura pale itapohitajika.

Kaunti hiyo ina wapiga kura 281,053 waliosajiliwa katika maneno sita: Baringo Kati, Baringo Kaskazini, Baringo Kusini, Mogotio, Eldama Ravine na Tiaty.

Wagombeaji wa kiti hicho ni Vincent Chemitei (UDA), Benjamin Chebon (TND), Shadrack Kibet Kaplawat (ARC), Steve David Kipruto (RLP), Samuel Letasio (KMM) na Daniel Kirui (Umoja na Maendeleo).

Katika Kaunti ya Nandi, Mkurugenzi wa IEBC Silas Rotich alisema tume iko tayari kuhakikisha uchaguzi mdogo wa Chemundu/Kapngetuny unafanyika kwa uwazi.

Zaidi ya maafisa 70 wamepata mafunzo ya siku nne kabla ya uchaguzi. Wagombeaji wanne wanashindana ambao ni David Kipchumba Too (TEP), Kiplimo Rutto (UDA), Kirwa Robert Kipchirchir, na Letting Shaffle Korir.
Jumla ya wapiga kura 14,535 wanatarajiwa kupiga kura katika vituo 30.

Katika eneobunge la Magarini, Kaunti ya Kilifi, baadhi ya wanasiasa wameanza kampeni za mlango kwa mlango baada ya kipindi rasmi cha kampeni kumalizika Jumatatu.

Walilenga hasa viongozi wa jamii, ambao wanatarajiwa kushawishi maamuzi ya wapiga kura.
Afisa Mkuu wa Uchaguzi Joseph Mwafondo alisema maandalizi kwa uchaguzi huo yamekamilika, akihakikisha zoezi la haki na uwazi kesho.

Ripoti na Gitonga Marete, George Munene, Manase Otsialo, Florah Koech, Barnabas Bii na Anthony Kitimo.
#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii