Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) imetangaza mpango wa kuboresha mitaala yake ili iendane na mabadiliko ya kasi ya sayansi na teknolojia, hatua inayolenga kuongeza ushindani wa wahitimu katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
Hayo yamebainishwa Mkoani Morogoro wakati wa mahafali ya tatu ya Taasisi hiyo, ambapo uongozi wa ICoT ulieleza kuwa licha ya mafanikio yaliyofikiwa, bado wanakumbana na changamoto ya upungufu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, hali inayochelewesha ubunifu na ufanisi katika utoaji wa elimu.
Akizungumza katika mahafali hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Karim Mkorehe alisema Wizara imejipanga kuhakikisha changamoto zote zinazohitaji ushiriki wa Serikali zinatafutiwa ufumbuzi wa haraka.
Aidha, aliutaka uongozi wa ICoT kutatua changamoto zilizo ndani ya uwezo wao ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Mahafali hayo yaliyofanyika Novemba 25 mwaka huu yalishuhudia jumla ya wahitimu 63 wakikabidhiwa vyeti katika fani mbalimbali za ujenzi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuandaa wataalamu waliobobea katika sekta muhimu ya miundombinu.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime