Ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Masuala ya Amani (SIPRI) yenye makao yake makuu nchini Sweden imesema Mauzo ya watengenezaji wakuu 100 wa silaha duniani yalifikia rekodi ya dola bilioni 679 kwa mwaka uliopita huku vita vya Ukraine na Gaza vikitajwa kuongeza mahitaji hayo.
Kwa mujibu wa SIPRI kiasi hicho kinaonekana kuwa cha juu kwa asilimia 5.9 kuliko mwaka uliopita ambapo katika kipindi cha 2015 hadi 2024, mapato ya watengenezaji 100 wakuu wa silaha yameongezeka kwa asilimia 26 huku matatizo ya uzalishaji huo yakiathiri usambazaji wa silaha hizo.
Katika taarifa hiyo, Lorenzo Scarazzato ambaye ni Mtafiti wa Programu ya Matumizi ya Kijeshi na Uzalishaji wa Silaha ya SIPRI, amenukuliwa akisema kuwa "Mwaka jana mapato ya silaha duniani yalifikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa na SIPRI, huku wazalishaji wakitumia fursa ya mahitaji makubwa.”
Katika hatua nyingine, Jade Guiberteau Ricard ambaye ni mtafiti wa programu hiyo hiyo, ameliambia Shiria la Habari la Ufaransa AFP kwamba imechochewa zaidi na Mataifa ya Ulaya, ingawa ‘maeneo yote yameongezeka isipokuwa Asia na Oceania na kusema ongezeko la mahitaji barani Ulaya linahusiana na vita vya Ukraine na mtazamo wa tishio la Urusi kwa nchi za Ulaya.
Taifa la Marekani ni makazi ya watengenezaji 39 kati ya 100 wakuu wa silaha duniani, wakiwemo watatu wa juu zaidi, Lockheed Martin, RTX (zamani Raytheon Technologies) na Northrop Grumman. Watengenezaji wa silaha wa Marekani walishuhudia mapato yao ya jumla yakipanda kwa asilimia 3.8 na kufikia dola bilioni 334 mwaka 2024, karibu nusu ya jumla ya dunia yote.
Wakati huohuo waandishi wa ripoti walibainisha kuwa matumizi ya bajeti kupita kiasi na ucheleweshaji vinatatiza programu kadhaa muhimu zinazoongozwa na Marekani, kama ile ya ndege ya kivita ya F-35 na manowari za Columbia-class.
Matokeo ya vita vya Ukraine kiuchumi yanaonesha kuwa Watengenezaji 26 kati ya 100 wakuu wa silaha walioko Ulaya ambao walishuhudia mapato yao ya jumla yakikua kwa asilimia 13 na kufikia dola bilioni 151. Watengenezaji wengine wanaonufaika na vita Hivyo ni kampuni Mbili kutokea Urudi huku kampuni tisa kati ya zile 100 kuu zikitokea Mashariki ya Kati.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime