Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameagiza kufunguliwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima na kupewa masharti maalumu ya kufuatiliwa kwa kipindi cha miezi sita, sambamba na kuelekeza taasisi zote za kidini kuandikiwa barua maalumu za kuwakumbusha mipaka ya ufanyaji kazi na wajibu wa kufuata sheria na katiba ya nchi.
Akizungumza hii leo wakati wa ziara yake katika mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Nchemba amesema kuwa ni muhimu kufanyika kwa mapitio mapya ya miiko, masharti na taratibu za uandikishwaji wa taasisi za kidini ili kuhakikisha zinazingatia misingi ya uendeshaji unaokubalika kisheria.
Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani kufuatilia kwa ukaribu taratibu za usajili, uendeshaji na ufuatiliaji wa taasisi zote za kidini, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha zinaendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria, katiba na masharti ya usajili.
“Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani, natambua uko hapa, fuatilia utaratibu mzuri, ziandike upya taasisi za kidini, miiko,masharti na uandikishwaji zile ambazo zilikuwa na shidashida wape uangalizi wa miezi sita,” alisema Dkt. Nchemba.
Aidha,amesema ziandikwe barua maalumu zitumwe kwa taasisi zote za kidini zikiwaelekeza kuzingatia mipaka ya ufanyaji kazi kulingana na sheria, katiba na masharti ya usajili.
“Ziandikie taasisi za kidini zote kuzikumbusha miiko na mipaka ya ufanyaji kazi kwa kufuata sheria, katiba ya nchi na masharti ya usajili,” alisisitiza.
Dkt. Nchemba alibainisha kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa taasisi za kidini katika kuimarisha maadili, kudumisha amani na mshikamano wa kijamii, lakini ni wajibu wake kusimamia utekelezaji wa sheria ili kulinda maslahi ya nchi na wananchi.
Waziri Mkuu amehimiza ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kidini katika kuendeleza amani, utulivu na maendeleo ya Taifa.
Na@MustaphaKinkulah
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime