Vijana 57 kati 61 wafutiwa kesi ya uhaini na DPP Mwanza

Vijana 57 kati ya 61 waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhaini, wamefutiwa mashtaka na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) leo, Jumatatu Novemba 24 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Ilemela, iliyopo Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Buswelu, mkoani Mwanza.

Kesi hiyo, yenye namba 26641/2025, ilisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Stella Kiama ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Safi Amani, aliwasilisha ombi la kufutwa kwa baadhi ya mashtaka na kueleza kuwa washtakiwa wanne waliobaki wataendelea na shauri hilo.

Vijana hao walikuwa miongoni mwa waliokamatwa na Jeshi la Polisi wakidaiwa kuhusika na maandamano ya 29 October yaliyosababisha vurugu, uharibifu wa mali, majeruhi na vifo katika maeneo mbalimbali nchini.

Hatua hii imejiri ikiwa zimepita siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumuagiza DPP kuwafutia kesi vijana waliojiingiza kwenye maandamano hayo kwa kufuata mkumbo, wakati wa hafla ya kumuapisha kwake iliyofanyika Jijini Dodoma.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii