Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa amezindua ugawaji wa vifaa vya umwagiliaji kwa wakulima wadogo ili kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika kilimo cha kisasa chenye tija na kuongeza uzalishaji.
Hafla hiyo imefanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi, kwa niaba ya wilaya zote za Mkoa wa Kagera Oktoba 26 mwaka huu.
Mhe. Mwassa amepongeza hatua hiyo, akieleza kuwa mpango huo utachochea maendeleo ya Sekta ya Kilimo kwa kuwasaidia wakulima wadogo, hususan wanawake na vijana wanaoishi katika maeneo yenye vyanzo vya maji na kuchangia usalama wa chakula nchini.
Aidha ameongeza kuwa jumla ya wakulima 634 kutoka halmashauri za Bukoba, Ngara na Muleba watanufaika na mpango huo ambapo watapatiwa vifaa vya umwagiliaji jozi 58.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania (TFSRP), Bw. Timothy Semguruka, amewataka wakulima watakaonufaika na vifaa hivyo kuvitumia kwa tija na kuvitunza kwa umakini ili viweze kuleta matokeo chanya katika uzalishaji wa mazao na maendeleo ya kilimo cha kisasa.
Uzinduzi wa kitaifa wa zoezi la ugawaji wa vifaa hivyo ulifanyika Oktoba 24 mwaka huu katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela vilivyopo Nzuguni, jijini Dodoma, ambapo vifaa hivyo vimetolewa kwa gharama ya shilingi bilioni 3.5 katika awamu ya kwanza.
Programu ya TFSRP inalenga kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali maji na kuimarisha kilimo cha uhakika katika maeneo yenye vyanzo vya maji nchini, ikiwa ni juhudi za Serikali kukuza uchumi wa kilimo na kuboresha maisha ya wakulima.