Matumizi sahihi ya Mbolea kuchochea agenda 10/ 30

Tathmini iliyofanyika hivi karibuni imeonesha kuwa matumizi ya mbolea nchini yamefikia wastani wa kilo 21 kwa hekta moja.

Hatua hii imechangiwa na juhudi za Serikali pamoja na mwamko mkubwa wa wakulima katika kuelekea kwenye uzalishaji wa kilimo cha kibiashara.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, upatikanaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 560,000 mwaka 2020 hadi kufikia tani 1,323,000 mwaka 2024/2025 ambapo Ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi.

Vilevile matumizi ya mbolea yamepanda kutoka tani 363,000 mwaka 2020 hadi kufikia tani 972,000 mwaka 2024. 

Katika kutekeleza Agenda 10/30,Serikali inalenga kuongeza matumizi ya mbolea kutoka wastani wa kilo 21 kwa hekta hadi kufikia kati ya kilo 30 na 40 kwa hekta ifikapo mwaka 2030. 

Hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji na tija katika mazao ya chakula na biashara, sambamba na kuhakikisha taifa linaendelea kujitosheleza kwa chakula.

Akizungumza na wakulima mkoani Songwe  Oktoba 22 mwaka huu katika mwendelezo wa Kampeni ya “Mali Shambani Silaha Mbolea”, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Maendeleo ya Mazao Bw. Samson Poneja ameeleza kuwa matumizi ya mbolea yameanza kupanda baada ya kudumu kwa muda mrefu katika wastani wa kilo 19 kwa hekta moja.

“Ongezeko hili linaonesha kuwa wakulima wanapata uelewa wa matumizi sahihi ya mbolea, jambo litakalosaidia kuongeza tija ya uzalishaji,” amesema Poneja.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kusisitiza matumizi ya mbolea kama nyenzo muhimu ya kuinua kilimo chenye tija na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii