Tamko la UDASA sio msimamo wa UDSM-Prof. Anangisye

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesema hakitambui wala kuhusika kwa namna yoyote na tamko lililotolewa na Jumuiya ya Wataaluma wa Chuo hicho (UDASA) Oktoba 23, 2025.

Akitoa taarifa hii, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Anangisye, amesisitiza kwamba UDASA ni jumuiya ya kitaaluma yenye uongozi na misimamo yake binafsi, ambayo haiwakilishi msimamo wa chuo.

“UDSM inaendelea kuwa taasisi ya umma inayozingatia misingi ya kitaaluma, Katiba, sheria za nchi na maadili ya umma, na kujikita katika mijadala yenye tija kwa maendeleo endelevu na mshikamano wa kitaifa,” amesema Prof. Anangisye.

Aidha, Prof. Anangisye ametoa wito kwa Watanzania wenye sifa kisheria kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa amani, utulivu na uzalendo, akibainisha kuwa hayo ndiyo msingi wa maendeleo na demokrasia.

Hii inakuja siku moja baada ya UDASA kutoa tamko kuhusu hali ya kiusalama nchini, ikisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za wananchi na maandalizi ya uchaguzi. Taarifa hiyo, iliyosainiwa na Mwenyekiti wa UDASA, Elgidius Ichumbaki, ilisisitiza kuwa ni muhimu kuchukua tahadhari mapema na kutafuta suluhu kwa njia ya amani.

“Tuweke kipaumbele katika kuifanya nchi yetu iwe salama na ya amani. Viongozi wetu watende haki, kwani amani haiwezi kuwepo bila watu kupata haki; tutende haki kabla ya kuhubiri amani,” imeeleza taarifa ya UDASA.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii