Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Yatoa TSh Bilioni 2.1 kwa Makundi Maalum

Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imetoa jumla ya shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya mikopo kwa makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Kitega Uchumi Cha Halmashauri ya Manispaa Kibaha, Kibaha Shopping Mall.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, ambaye alipongeza jitihada za wajasiriamali wa Kibaha kwa kuendelea kujihusisha na shughuli za kiuchumi zinazochangia maendeleo ya Manispaa hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Dkt. Shemwelekwa amesema kuwa Manispaa ya Kibaha imetoa mikopo hiyo kwa lengo la kuwawezesha wananchi kujiajiri na kukuza kipato chao, sambamba na kutekeleza agizo la Serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Tunataka kila mwananchi wa Manispaa ya Kibaha awe na shughuli halali ya kujipatia kipato. Mikopo hii haina riba — ukikopa milioni moja, unarudisha milioni moja.

Lengo letu ni kuinua uchumi wa wananchi na kuepusha utegemezi wa mikopo yenye riba kubwa maarufu kama kausha damu,” alisema Dkt. Shemwelekwa.

Aidha alibainisha kuwa zaidi ya watu 3,600 watanufaika na mikopo hiyo na kuwataka wanufaika kuitumia vyema ili kukuza biashara zao na kuongeza kipato cha kaya.

Kwa upande wao baadhi ya wajasiriamali walioshiriki hafla hiyo wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mikopo hiyo nafuu, wakisema awali walilazimika kukopa kutoka taasisi binafsi zenye masharti magumu na riba kubwa, hali iliyokuwa ikikwamisha ukuaji wa biashara zao.

Hafla hiyo pia iliambatana na mafunzo maalum kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo wataalamu kutoka Manispaa walitoa elimu kuhusu usimamizi wa mikopo, ujasiriamali na utunzaji wa kumbukumbu za fedha. Vikundi vilivyomaliza mafunzo vilikabidhiwa vyeti vya kutambua ushiriki wao.

Dkt. Shemwelekwa alihitimisha kwa kuwataka wanufaika kuwa mfano wa mafanikio ili mikopo hiyo iendelee kunufaisha wananchi wengine zaidi katika Manispaa ya Kibaha.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii