Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron leo atakutana na washirika wake wa Ulaya kujadili juu ya ujumbe wa kijeshi nchini Mali. Maafisa wa serikali wamesema Macron atatangaza ikiwa anawaondoa wanajeshi wa Kifaransa kutoka Mali. Kuondolewa na vikosi vya Ufaransa kutoka Mali kulikuwa kumetarajiwa kwa miezi kadhaa na pia kutahitimisha kikosi kazi cha Takuba kilichoandaliwa na Ufaransa. Hatua hiyo huenda ikaibua wasiwasi juu ya mustakabali wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa sambamba na ule wa Umoja wa Ulaya katika ukanda wa Sahel. Hata hivyo Ufaransa ilikuwa tayari imesema kuwa itaendelea kushirikiana na washirika wake nchini Mali. Vikosi vya Ufaransa vimekuwepo Mali tangu mwaka 2013. Endapo vitaondolewa vinaweza kupelekwa katika nchi nyingine za ukanda huo. Niger na Burkina Faso zimekuwa zikilengwa katika mashambulizi ya wanajihadi yaliyoanzia Mali.